Jioni ya tarehe 17 Agosti, “Maelfu ya Maili kwenye Njia ya Hariri · Rangi za Afrika”, onyesho la taa za ndege zisizo na rubani (Drone Light Show), ambalo ni programu maalum ya Mwaka wa 2026 wa China na Afrika wa Mabadilishano ya Watu kwa Watu, lililoandaliwa na Shaanxi Radio and Television Media Convergence Group, lilifanyika kwa mafanikio jijini Dar es Salaam.Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, pamoja na wananchi wa China na Tanzania kutoka sekta mbalimbali, walihudhuria hafla hiyo.
Balozi Chen alibainisha kuwa maonesho ya usiku wa leo si tu burudani ya kuvutia kwa macho inayotumia teknolojia ya kisasa, bali pia ni mazungumzo ya moyo kwa moyo kati ya China na Afrika yanayovuka milima na bahari. China iko tayari kushirikiana na Tanzania kutumia Mwaka wa 2026 wa China na Afrika wa Mabadilishano ya Watu kwa Watu pamoja na maadhimisho ya miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika kama fursa ya kuendeleza urafiki wa jadi, kuimarisha kujifunza kwa pamoja kati ya ustaarabu, na kuleta manufaa zaidi kwa wananchi wa pande zote mbili.
Zikimulika angani wakati wa usiku, drone 500 ziliunda miundo 12 ya kipekee, ikiwemo bendera za taifa za China na Tanzania pamoja na Reli ya TAZARA, zikionesha kwa uhalisia urafiki wa kina na ushirikiano wenye matunda kati ya mataifa hayo mawili. Ukumbi wa hafla ulijaa shangwe na makofi, huku watazamaji wakirekodi matukio hayo yenye kuvutia, wakitazamia kwa pamoja mustakabali mzuri zaidi kwa China na Afrika.