Mnamo Juni 24, Ubalozi wa China na Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania waliandaa kwa pamoja hafla ya kuonesha filamu kwa ajili ya kuadhimisha miaka 30 ya Ushirikiano wa Kimkakati wa Uratibu kati ya China na Urusi, pamoja na miaka 25 tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Ujirani Mwema na Ushirikiano wa Kirafiki kati ya nchi hizo mbili.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mheshimiwa Andrey Avetisyan, pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Mheshimiwa Paul Makonda. Zaidi ya watu 200 kutoka makundi mbalimbali ya jamii walishiriki katika tukio hilo.
Katika hotuba yake, Balozi Chen alielezea kwa kina Ushirikiano Kamili wa Kimkakati wa Uratibu kati ya China na Urusi katika Enzi Mpya, na kusisitiza kuwa China iko tayari kushirikiana na Urusi na Tanzania kuimarisha ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote na matokeo ya ushindi kwa wote. Pia alisema China itaendelea kuwa mtetezi wa usawa na haki duniani pamoja na mshirika wa maendeleo na ustawi wa mataifa.
Kwa upande wake, Balozi Avetisyan alisifu kwa kiwango cha juu uhusiano kati ya Urusi na China, akisema kuwa Urusi itafanya kila linalowezekana kuendeleza zaidi ushirikiano wa kimkakati na ujirani mwema kati ya nchi hizo mbili kwa ajili ya maendeleo ya pamoja, pamoja na kudumisha usalama na utulivu wa dunia.
Naye Waziri Makonda alisema kuwa Tanzania, China na Urusi zina historia ndefu ya mahusiano ya kirafiki, na akaeleza matarajio yake kwamba pande hizo tatu zitaendelea kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali.
Katika hafla hiyo, filamu ya pamoja ya China na Urusi iitwayo “Hariri Nyekundu (Red Silk)” ilioneshwa. Filamu hiyo inasimulia hadithi ya mjumbe wa Chama cha Kikomunisti cha China ambaye, kwa ulinzi wa maafisa wa ujasusi wa Umoja wa Kisovieti, alifanikiwa kupeleka nyaraka muhimu hadi Moscow.
