Tarehe 24 Mei, Ubalozi wa China nchini Tanzania uliandaa Kongamano la Utamaduni la “Maritime Silk Road Impression: Tea for Harmony Yaji” jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mazungumzo kati ya Tamaduni.
Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian, na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Mhe. Paul Makonda, walihudhuria hafla hiyo. Wengine waliohudhuria ni pamoja na Mhe. Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na zaidi ya watu 100 wakiwemo mabalozi, wanadiplomasia na wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.
Katika hotuba yake, Balozi Chen alikumbushia historia ya mabadilishano ya watu kwa watu kati ya China na Afrika pamoja na China na Tanzania katika muktadha wa Barabara ya Hariri ya Baharini (Maritime Silk Road). Alisema kuwa China itatumia Siku ya Kimataifa ya Mazungumzo kati ya Tamaduni kama fursa ya kuendeleza roho ya Barabara ya Hariri, kuimarisha kujifunza na kubadilishana uzoefu kati ya tamaduni mbalimbali, kujenga daraja pana zaidi la mawasiliano ya watu kwa watu kati ya China na dunia nzima, na kutoa msukumo wa kudumu katika kujenga jumuiya ya karibu zaidi ya China na Tanzania pamoja na China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja.
Waziri Makonda alikubaliana na umuhimu wa mazungumzo kati ya tamaduni mbalimbali na kusema kuwa Tanzania inathamini mchango wa China. Alieleza kuwa Tanzania inatarajia kuimarisha zaidi ushirikiano, kukuza mabadilishano ya kitamaduni na kuhifadhi urithi wa pamoja kwa manufaa ya binadamu wote.
Wageni waliohudhuria hafla hiyo walifurahia maonesho ya urithi wa utamaduni usiogusika wa China, yakiwemo maonesho ya ala ya jadi ya guqin, utamaduni wa kufurahia ubani, sanaa ya porcelaini na sherehe ya chai ya Kichina. Aidha, kulikuwa na maonesho ya ngoma za jadi za China na Tanzania.