Mwanzo > Habari kuhusu China
Jacqueline Liana: Maajabu ya mpango wa China wa GSI katika utatuzi wa migogoro kimataifa
2025-04-10 19:37

Na Jacqueline Liana

USALAMA na maendeleo ni hali pacha zinazotegemeana mithili ya mbawa za ndege, bawa moja likiwa na hitilafu ndege hawezi kuruka. Ustawi wa binadamu unahitaji usalama na amani kwa maendeleo endelevu katika kila nyanja ya maisha yake.

Mataifa yakiwa na sera zinazotekelezwa kwa ajili ya kupigania na kuimarisha  usalama, matokeo yake ni kupatikana kwa maendeleo kwa jumuiya ya wanadamu.

China ni taifa lililopita katika historia ngumu iliyohusisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilevile kupigana kujihami dhidi ya uvamizi wa nchi yao uliofanywa na mataifa mengine.

Kwa historia hiyo, haishangazi kusikia taifa hilo kwa sasa likiwa mstari wa mbele likihubiri usalama na amani miongoni mwa mataifa, pasipo kujali udogo au ukubwa wa nchi.

Wahenga walisema historia ni mwalimu mzuri; hakika China imejifunza thamani ya amani  kwa maisha ya binadamu na maendeleo yake baada ya kupita katika vipindi vigumu.

Rais Xi Jinping wa China, Aprili 21, 2022, alipendekeza Mpango wa Usalama wa Kimataifa (GSI) katika kukabiliana na changamoto za usalama duniani.   

Mpngo wa GSI unalenga kukabili visababishi vikuu vya migogoro ya kimataifa, kuimarisha utawala wa usalama wa kimataifa na kustawisha amani na maendeleo ya kudumu duniani.

China inaweka mkazo wa kuzingatiwa malengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN) tangu vilipomalizika Vita vya Pili vya Dunia.

Mpango wa GSI unafafanua malengo na madhumuni ukionyesha umuhimu wa mataifa kuwa na tafakuri ya pamoja ya mara kwa mara kuhusu madhila yaliyosababishwa na vita hivyo, hadi makubaliano ya kuunda UN.

Wakati wote, kwa mujibu wa GSI, mataifa yanapaswa kuzingatia kanuni za usalama za usawa, kuwa na mifumo ya usalama yenye uwiano, ufanisi na endelevu.

Mpango GSI unasisitiza kwamba usalama unatakiwa kuwepo kwa kila taifa, wala  isiwepo nchi ambayo itatafuta kuimarisha usalama wake kwa gharama ya usalama wa nchi nyingine.

Kwa uongozi thabiti wa Rais Xi Jingping, serikali ya China imepiga hatua katika kutekeleza GSI, kitaifa, kikanda na kimataifa.

Ni sahihi kusemwa pasi na shaka kwamba GSI imebeba kwa uzito unaostahili ajenda ya kuhakikisha dunia inakuwa mahali salama kwa jamii ya wanadamu wote pasipo ubaguzi.

UFANISI WA GSI KIMATAIFA

Tangu kuasisiwa kwa GSI utekelezaji wake umeonekana katika kutatua migogoro kwenye mataifa ya Afrika, pia umekuwa maarufu Asia ya Kusini-Mashariki, Mashariki ya Kati, Amerika ya Kusini hadi Visiwa vya Pasifiki.

Mpango wa GSI mkubwa umepongezwa na kupokewa na jumuiya ya kimataifa, ambapo nchi na mashirika ya kimataifa yameuunga mkono kwa sababu ni njia yenye tija.

Kupitia mpango huo, China imetumia diplomasia ya upatanishi na kufanya juhudi zisizo na kikomo kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya kisiasa.

Miongoni mwa migogoro hiyo imo ambayo ni sugu ikiwa ni pamoja na suala la nyukilia la Iran, vitisho vya kiusalama katika Peninsula ya Korea, vita vinavyoendelea sasa kati ya Russia na Ukraine, suala la Syria, mgogoro wa kihistoria wa Israel na Palestina na suala la Afghanistan.

Novemba mwaka jana, Rais Xi Jingping, alituma salamu za pongezi kwa maadhimisho maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina.

Pia, Novemba 29,  Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi ambaye pia ni Mjumbe Idara ya Mambo ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), aliongoza kikao cha ngazi ya juu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa Palestina na Israel, kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York.

Katika kikao hicho, Wang, aliwasilisha waraka wa mapendekezo matano ya  China juu ya kusuluhisha mgogoro wa Palestina na Israel, na Novemba 21 Rais Xi Jingping alihudhuria mkutano wa viongozi wa nchi zinazounda  BRICS kuhusu hali ya Mashariki ya Kati hasa Gaza.

Katika mkutano huo, Rais Xi Jingping aliainisha mambo matatu ikiwa ni suluhisho la mgogoro wa Gaza; kwanza,  pande zinazohusika katika mzozo huo zikomeshe uhasama na kusitisha mapigano mara moja pamoja na kukomesha ghasia dhidi ya raia; pili, njia kwa ajili ya misaada ya  kibinadamu zilindwe bila kizuizi; tatu, jumuiya ya kimataifa ichukue hatua kwa vitendo kuzuia mzozo kuvuka mipaka.

Ufanisi wa GSI umezaa matunda mazuri ambapo ulifanikisha kupatikana kwa makubaliano ya amani kati ya Ufalme wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, chini ya upatanishi wa China.

Mafanikio hayo ya GSI ni mfano wa namna nchi zinavyoweza kutatua mizozo na tofauti kwa kuzungumza na kushauria ili kuendelea kuwa majirani wema. 

Hivi karibuni, Rais Xi Jinping alizungumza kwa simu na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy na kumwambia China itaendelea kuwezesha mazungumzo ya amani na kufanya juhudi za kusitisha vita kati ya Ukraine na Russia.

Kupitia GSI, China iliwezesha kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa amani  ya katika Pembe ya Afrika ambao ulimalizika kwa kufikia makubaliano muhimu kuhusu usalama na amani.

China ilifanikiwa kufanya kongamano la pili la usalama la Mashariki ya Kati na kutoa pendekezo lenye vipengele vinne kwa ajili ya kuimarisha usalama katika eneo hilo.

KWANINI USALAMA WA MATAIFA

Sababu ya China kutafuta usalama miongoni mwa mataifa ni ukweli dhahiri kwamba maendeleo ya nchi kubwa ama ndogo hayawezi kupatikana bila hali ya usalama.

Katika kuonyesha nia njema kwa usalama wa dunia, China ni nchi ambayo inaonyesha kwa vitendo dhamira ya dhati ya kutaka usalama wa mataifa kwa ajili ya amani na maendeleo.

China ambayo ni mchangiaji mkuu wa wanajeshi wa kulinda amani kati ya wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pia ni nchi pekee ya kwanza kati ya mataifa matano ya yenye silaha za nyukilia ambayo imetoa ahadi ya kutotumia silaha hizo katika migogoro.

Taifa hilo linashikilia kwa dhati makubaliano kwamba "vita vya nyukilia haviwezi kushinda na havipaswi kupiganwa kamwe". Rais Xi Jingping amesisitiza mara kwa mara kuwa, silaha za nyuklia hazipaswi kutumiwa na vita vya nyukilia haipaswi kupiganwa.

Serikali ya China imetia saini zaidi ya mikataba 20 ya kimataifa ya udhibiti wa silaha, na kusukuma kuhitimishwa kwa taarifa ya pamoja kati ya nchi vinara wa silaha za nyukilia inayozuia matumizi yake katika vita.

China ya kisasa, kupitia GSI itaimarisha nguvu ya usalama wa dunia na haki ya kimataifa pasipo kujali kiwango cha maendeleo kimefikiwa na taifa hilo, kamwe haiwezi kukandamiza wala kujitanua dhidi ya mataifa mengine.

China ina mipango mitatu muhimu ambayo inanufaisha jumuiya ya kimataifa; Mpango wa Maendeleo wa Kimataifa (GDI), Mpango wa Ustaarabu wa kimataifa (GCI) na GSI yenyewe.

China,  ambayo kwa sasa ni miongoni mwa mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani, inaheshimu historia ya mwanadamu inayostawi  ikifungamanishwa na usalama, ustaarabu kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Usalama ndiyo msingi wa maendeleo, maendeleo ndiyo yanachochea usalama na ustaarabu; hivyo kufanya GDI, GCI na GSI  kuwa nguzo muhimu kwa jamii ya kimataifa yenye mustakabali wa pamoja unaokumbatia ubinadamu.

Masilahi ya wanadamu katika dunia hayana budi kujikita katika umoja, usalama na amani, badala ya kugawanyika na kuishi katika hali tete za uhusiano wa kutoaminiana na uhasama.

Mpango wa GSI ni ufumbuzi unaofaa unaojibu swali la dhana gani inaweza kutumika kwa ajili ya kuhakikisha dunia inakuwa mahali salama kwa binadamu kujiletea maendeleo.

Kwa mujibu wa ripoti ya utekelezaji wa GSI kwa mwaka 2024, ni kwamba mpango huo umepata mafanikio ya kutia moyo kitaifa, kikanda na kimataifa takribani katika mabara yote.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, China imekuwa ikifanya kazi na mataifa pamoja na mashirika ya kitaifa, kikanda na kimataifa kukuza ushirikiano wa usalama chini ya mpango wa GSI.

Taasisi ya Utafiti wa Kimataifa ya China (CII) na Kituo cha Mafunzo ya Mpango wa Usalama wa Kimataifa ndizo zimefanya utafiti maalumu kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa GSI.

Ripoti hiyo inaeleza suala la usalama linahusu amani na maendeleo ya mwanadamu na mustakabali wake, huku ikisisitiza taifa moja haliwezi kusababisha ukosefu wa usalama kwa taifa lingine kwa ajili ya taifa hilo kuwa salama.

Inaeleza dunia kwa sasa inapita katika mabadiliko ya kasi katika kila nyanja ya maisha, ambayo hayajawahi kuonekana kwa karne moja huku matukio ya migogoro kwa sababu mbalimbali ikiongezeka.

“Dunia imeingia katika kipindi kipya cha misukosuko na mabadiliko. Hali ya usalama duniani imekuwa ya kutatanisha sana, huku kukiwa na ongezeko la matukio makubwa yanayoathiri usalama na hayakabiliwi kwa wakati kunusuru wanadamu.

Jumuiya ya kimataifa inakabiliwa na hali ya ukosefu wa usalama tangu kumalizika kwa vita baridi, huku upungufu wa amani, maendeleo, usalama na unaoongezeka,” ripoti imeeleza.

China ikiwa ni mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), yenye kura ya turufu, katika mpango GSI inafanya kazi na Umoja huo kuona unasimamia amani ya dunia kwa mujibu wa katiba yake na kuanzishwa kwake kwa kutekeleza kanuni zake za usalama kwa usawa.

...kuzingatia maono ya usalama wa pamoja, kwa mapana yake, kwa ushirikiano endelevu wa kutetea utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo, kushauriana na kuunga mkono juhudi zote zinazofaa zenye kukabiliana na migogoro pasipo madhara ya kibinadamu,” ilieleza ripoti hiyo.

Katika mkutano wa wakuu wa nchi za China na Uarabuni, Rais Xi Jinping alitamka bayana kwamba China inazikaribisha nchi za Uarabuni kushiriki katika GSI na itaendelea kuchangia kile alichosema ni “hekima ya Wachina katika kukuza amani na utulivu katika Mashariki ya Kati.

Rais Xi alisema China iko tayari kufanya kazi na mataifa kutekeleza GSI, kukuza utatuzi wa mizozo ya kimataifa kupitia mazungumzo na mashauriano, na kuhimiza usuluhishi wa kisiasa.

Mpango wa GSI unatoa wito kwa nchi kurekebisha hali ya kimataifa inayobadilika katika moyo wa mshikamano na kushughulikia changamoto tata na zilizofungamana za usalama kwa kuzingatia dhana ya kila upande kufaidika.

Unalenga kuondoa visababishi vikuu vya migogoro ya kimataifa, kuboresha utawala wa usalama duniani, kuhimiza juhudi za pamoja za kimataifa ili kuleta utulivu.

Mpango huo ni mawazo madhubuti yanayobuni njia mpya ya mataifa kufuata katika  kuziba mianya inayosababisha ukosefu wa amani na   kukabiliana na changamoto za kiusalama duniani ili kufikia utulivu na usalama wa kimataifa.

Hivyo basi, inaweza kuelezwa kwamba GSI ni dira ya amani, maendeleo, na ushirikiano wenye kujumuisha lengo na mahitaji la kujenga jumuiya ya kimataifa yenye mustakabali wa pamoja kwa wanadamu.

Katika kutekeleza GSI, China imeendelea kuweka uwiano kati ya maendeleo na usalama, kuweka maendeleo katika kiini cha ajenda yake ya kimataifa, na kufanya kazi ili kuimarisha usalama endelevu kupitia maendeleo endelevu.

USALAMA WA AFRIKA

Kwa kuwa ni dhahiri dunia inakabiliana na maeneo yenye migogoro kutokana na sababu mbalimbali; ya kikanda na kimataifa kunahitajika   amani badala ya vita, uaminifu badala ya mashaka, umoja badala ya mifarakano na ushirikiano badala ya kutunishiana msuli.

China inafanya kazi kwa bidii kutafuta suluhu zenye sifa za Kichina kwenye masuala muhimu, kuendeleza mazungumzo ya amani, na kujitahidi kupata suluhu za kisiasa.

Mathalani, mzozo wa Ukraine na Russia, China ipo katika msimamo wa haki na kuhimiza mazungumzo ili amani ipatikane ambapo Februari 2023, ilitoa waraka wenye kichwa cha habari "Msimamo wa China juu ya Usuluhishi wa Kisiasa wa Mgogoro wa Ukraine", ukibeba mapendekezo 12.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuheshimu mamlaka za nchi zote, kuacha fikra za vita baridi, kuacha uhasama, kuanzisha mazungumzo ya amani na kupunguza hatari za kimkakati.

Katika kuendeleza uhusiano wake na mataifa ya Afrika, China imesimama katika kanuni ya kuaminiana na mshikamano kwa ajili ya maslahi mapana ya pande zote.  

Kupitia mpango wa GSI, China imeunga mkono nchi za Kiafrika katika masuala ya usalama kwa kutoa msaada wa kuisaidia Afrika kuondokana na  vitisho dhidi ya amani, usalama na utulivu wake.

Agosti 2023, Rais Xi Jingping, katika mkutano wa viongozi wa China na Afrika alisema  China iko tayari kufanya kazi na Afrika katika kutekeleza maono mapya ya usalama wa pamoja.

Chini ya mpango wa GSI, China imeimarisha ushirikiano na Afrika katika sera na maono na kutekeleza kikamilifu ushirikiano wa usalama, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kijeshi kwa Umoja wa Afrika, kushirikiana kikamilifu katika udhibiti wa silaha ndogo ndogo na nyepesi.

Pia, kuziunga mkono kwa dhati nchi za Afrika katika kudumisha usalama wa kikanda na kupambana na ugaidi.

China ilikuwa mwenyeji wa kongamano la pili na la tatu la amani na usalama kati ya China na Afrika mwaka 2022 na 2023, na kujenga maelewano kuhusu ushirikiano na kuimarisha mawasiliano ya kimkakati kati ya idara za ulinzi za China na Afrika.

China imeiunga mkono kikamilifu Afrika katika juhudi zake za kukabiliana na changamoto za kiusalama, huku ikiendelea kutekeleza mtazamo wa amani na maendeleo katika pembe ya Afrika.

Mjumbe maalumu wa mambo ya pembe ya Afrika wa wizara ya mambo ya nje ya China alifanya ziara saba barani Afrika katika muda wa miaka miwili.

Katika barua yake ya pongezi kwa jukwaa la pili la amani na usalama la China na Afrika, Rais Xi Jingping alibainisha kuwa China siku zote imekuwa ikifanya kazi ya kuendeleza uhusiano na Afrika, kuchukua njia sahihi ya urafiki.

Aliandika kwamba hilo linafanyika kwa kuzingatia masilahi ya pande zote, uaminifu, upendo na nia njema, na kwamba China itashirikiana na Afrika kulinda mfumo wa kimataifa na kudumisha umoja wa mataifa na utekelezaji wa haki kati ya nchi hizo mbili.

“Kujenga jumuiya ya China -Afrika yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya,” alisema kiongozi huyo.   

China, likiwa ni taifa kubwa, na mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inabeba jukumu la kudumisha utulivu wa kimkakati wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu ya dunia.

Suala la usalama linahusu amani na maendeleo ya dunia, na mustakabali wa binadamu. Hivi sasa ulimwengu unapitia mabadiliko ya kasi ambayo hayahawahi kuonekana katika karne moja.

 Hali ya usalama duniani imekuwa ya kutatanisha na inaleta  wasiwasi kuhusu mataifa yalivyogawanyika na kusababisha wasiwasi wa usalama unaoathiri maendeleo.

Ni dhahiri kwamba, tangu kumalizika kwa vita baridi, jumuiya ya kimataifa imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa amani, maendeleo na usalama.

Maswali ya aina gani ya dhana ya usalama ambayo mataifa yanahitaji ili kufikia usalama wa pamoja, yamekuwa masuala ya dharura ya nyakati hizi hivyo kuhitajika ufumbuzi unaofaa.

Mpango wa GSI ni dhana ambayo inaalika mataifa kushiriki katika kuhakikisha usalama wa wanadamu kwa ajili ya maendeleo popote walipo.

HEKIMA YA WACHINA

 Rais Xi Jingping aliwahi kusema kwamba kupitia GSI, China itaendelea    kuchangia hekima ya Wachina katika kukuza amani na utulivu duniani na kwamba ipo tayari kufanya kazi na kila mdau kutekeleza GSI katika utatuzi wa mizozo ya kimataifa kwa njia ya mazungumzo, kushauriana na kuhimiza suluhu ya kisiasa ya mizozo ya kimataifa.

Ili kufikia amani ya kudumu ya dunia na kujenga jumuiya ya kimataifa yenye usalama kwa wote, China imeendelea kutumia vyema majukwaa ya mazungumzo kwa ajili ya kubadilishana usalama wa kimataifa.

 Ili kufikia amani ya kudumu ya dunia na kujenga jumuiya ya usalama kwa wote, China imeshiriki katika ushirikiano wa pande mbili na wa kimataifa wa usalama na pande mbalimbali chini ya mpango wa GSI.

Hakika, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, China imeongeza kimataifa, mabadiliko ya mawazo na mawasiliano ya kisera kuhusu masuala ya usalama wa kimataifa kupitia vikao na majukwaa ya mazungumzo.

Ifahamike kuwa, sera ya mambo nje ya China kamwe si ya chokochoko au kujipanua kimaeneo, kamwe haitafuti ubabe, bali inabaki kuwa nguvu thabiti ya kudumisha amani na utulivu wa kikanda na kimataifa kwa jumla.

Uwepo wa mpango wa GSI na utekelezaji wake ili kupata majibu ya migogoro sugu na iliyoibuka hivi karibuni miongoni mwa mataifa ni uthibitisho wa utekelezaji wa sera hiyo.

Kwa kuangalia matokeo ya utekelezaji wa GSI, tangu ulipoasisiwa mwaka 2022 hadi sasa, inaweza kuhitimishwa kwa kusema umezaa matunda ya kufurahisha kwa usalama na maendeleo endelevu ya binadamu duniani.

MWISHO


Suggset To Friend:   
Print