Mwanzo > Habari kuhusu China
CCM kuboresha misingi ya Ujamaa na kujitegemea
2014-07-04 20:50

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema kitaendelea kuboresha misingi ya Ujamaa na Kujitegemea ikiwa ni mwendelezo wa jitihada zake za kuleta maendeleo na usawa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana baada ya semina na Makamu wa Rais wa China Li Yuanchao, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Phillip Mangula alisema uboreshaji wa utawala kwa misingi ya ujamaa ni jambo endelevu.

Alisema CCM imeleta mabadiliko ya haraka kwa wananchi hivyo ujamaa ni njia mbadala ya kuleta usawa na maendeleo.

Makamu mwenyekiti huyo aliongeza kuwa ujamaa wa sasa umebadili muundo wake kwa kuwamilikisha watu rasilimali ili washiriki kikamilifu kuleta maendeleo badala ya kuitegemea Serikali.

Alipoulizwa inawezekanaje kufanya ujamaa wakati Tanzania ni tegemezi kwa nchi zinazoamini mfumo wa kibepari, Mangula alisema utegemezi utaisha iwapo ujamaa ‘mpya’ utatekelezwa ipasavyo.

“Tukitekeleza ujamaa haya mambo ya utegemezi yataisha. Tunachokubaliana wote ni misingi ya ujamaa ya umiliki wa umma ambao kwa sasa umebadilika kutoka kwa Serikali kwenda kwa wananchi,” alisema Mangula.

Ikumbukwe kuwa falsafa na sera za ujamaa nchini zilianguka baada ya Serikali kukubali masharti ya kibepari ya kuendesha uchumi kutoka kwa mashirika ya fedha ya kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB) mwishoni mwa miaka ya 1980.

 

Na Nuzulack Dausen, Mwananchi

Posted  Jumatano,Juni25  2014

Suggset To Friend:   
Print