Mwanzo > Habari kuhusu China
Dk Bilal aipongeza China
2014-07-04 20:48

MAKAMU wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuimarisha uchumi wake, kutokana na kutegemea nguvu kazi ya watu wake, tofauti na nchi nyingine zilizoendelea zinazojinufaisha kutokana na kuwanyonya wengine.

Dk Bilal alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa Taasisi ya Confucius ya China, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na washiriki mbalimbali wa Afrika.

“Kihistoria, nchi nyingi zilizoendelea zimepata utajiri wake kwa kutawala na kuzinyonya nchi nyingine, hali ambayo ni tofauti kwa nchi ya China ambayo imepata mafanikio yake kutokana na jitihada za watu wake,” alisema.

Alitoa changamoto kwa nchi za Afrika kufuata mkondo wa kujipatia maendeleo wa China, kutokana na ukweli kuwa nchi hiyo pamoja na bara zima la Asia, nayo kwa kipindi kirefu ilikabiliana na matatizo ya kiuchumi kama ilivyo sasa kwa Afrika.

Aliongeza kuwa kwa sasa si lazima Afrika, ifikirie kuanza na hatua kubwa kama vile kutuma ndege aina ya roketi mwezini, bali inaweza kuanza kwa kuzalisha bidhaa kwa ajili ya mahitaji ya watu wake na za kuuza nje.

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa China, Li Yuanchao, alisema ana uhakika taasisi hiyo ya Confucius iliyopo Afrika nzima, itasaidia kukuza masuala ya uchumi na utamaduni baina ya China na Afrika. Aidha, aliagiza taasisi hiyo ijikite katika kutoa mafunzo ya utaalamu mbalimbali na kutoa ajira.

“Si tu mtoe mafunzo ya lugha ya kichina pekee na utamaduni, lakini pia saidieni jamii inayowazunguka kukuza maendeleo yao, kama vile msemo wa kichina unavyosema kuwa usimpatie rafiki yako samaki tu, bali mfundishe juu ya namna ya kumvua samaki huyo,” alisisitiza Yuanchao.

Suggset To Friend:   
Print