Mwanzo > Habari kuhusu China
China kuwafunda wanamichezo wa Madola
2014-03-11 02:37

SERIKALI ya China imekubali kuendesha mafunzo kwa wanamichezo 30 wa Tanzania wanaotarajiwa kuiwakilisha Tanzania kwenye michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola inayotarajia kufanyika Glasgow, Scotland kuanzia Julai 23 –Agosti 3 mwaka huu.

Taarifa ya kitengo cha mawasiliano cha Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilisema, Tanzania na China pia zimekubaliana kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia unaoendelea kuimarika kila mwaka, hususan kwa sasa nchi hizo zinaposherehekea miaka 50 ya ushirikiano.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makubaliano hayo yalifanyika wakati Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Benard Membe alipokutana na waziri wa China, Wang Yi mjini Beijing wiki iliyopita kuzungumzia masuala yanayohusu maeneo ya ushirikiano wa nchi zao.

Wang Yi alisema, ushirikiano baina ya nchi hizi ni wa kidugu na hivyo Serikali ya China itaendelea kusaidia kwa hali na mali miradi waliyoahidi kwa maendeleo ya Tanzania na watu wake.

Membe, ambaye alikuwa China kwenye ziara ya siku tano, aliahidi kuratibu Wizara na Taasisi za Serikali zinazohusika na miradi ya ushirikiano ili kuhakikisha matunda ya miradi hiyo yanaonekana.

Membe alisema, China ni marafiki wa Afrika lakini ni marafiki wa karibu wa Tanzania hivyo sherehe za miaka 50 ya uhusiano huo zidhihirishwe na miradi ya mafanikio ambayo nchi zote mbili zimekubaliana kwa maendeleo ya watu wake.

Mbali na misaada ya vifaa mbalimbali vya ujenzi na huduma za maji na afya, hadi sasa Serikali ya China imekamilisha miradi mikubwa ya ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, ukarabati wa Uwanja wa Amaan Zanzibar, ujenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ifakara, na ujenzi wa shule mbalimbali.

Miradi mingine kadhaa inaendelea sasa ukiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Miradi mingine mingi iko kwenye majadiliano kama vile ujenzi wa jengo la Wizara ya Mambo ya Nje, awamu ya pili ya Mkongo wa Taifa, Nishati ya Umeme wa Upepo Singida, Bandari ya Mbegani Bagamoyo na ukarabati wa Reli ya TAZARA.

Akiwa kwenye ziara hiyo, Membe pia alikutana na Makamu wa Rais wa China, Li Yuanchao ambaye alielezea China inaitazama Tanzania kama mshirika mwenza kwenye maendeleo, hivyo uhusiano wa nchi hizo una manufaa sawa kwa pande zote mbili.

Alisema ukuaji wa uchumi wa nchi nyingi za Kiafrika umesababisha Serikali yake kushawishi wawekezaji wengi kuwekeza Afrika, lakini hali ya usalama na utulivu nchini Tanzania inawavutia wengi kuwekeza zaidi huko.Membe na ujumbe wake pia walikutana na kufanya mzungumzo na Makamu Waziri wa Biashara, Li Jinzao ambapo aliainisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na China kwa sasa.

Jinzao alisema, mbali na miradi mingi inayoendelea kwa sasa mradi wa kukarabati Reli ya TAZARA unapewa kipaumbele na Serikali ya China kwani ndio mradi wa kwanza baina ya nchi hizi mbili.

 

HABARI LEO, 6TH MARCH 2014

Suggset To Friend:   
Print