Mwanzo > Rolling News Report
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
2017-06-13 20:56
Simu : +255-22-2114512, 2116898
Email : press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA

Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake, kwa bajeti nzuri iliyowasilishwa jana tarehe 08 Juni, 2017 Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango.

Mhe. Dkt. Lu Youqing ametoa pongezi hizo leo tarehe 09 Juni, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli ambapo amesema bajeti iliyowasilishwa imeakisi dhamira ya kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ujenzi wa viwanda.

Ameongeza kuwa pamoja na kuwasilishwa kwa bajeti nzuri, uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara na hivyo kuwavutia wadau wengi wa maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambao wamekuwa wakishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na yenye umuhimu mkubwa.

Mhe. Dkt. Lu Youqing amebainisha kuwa Tanzania ni mahali pa kipaumbele kwa uwekezaji kutoka China na kwamba Serikali ya China itaendelea kuwashawishi wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa nchini ili kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kuzalishaji ajira nyingi zaidi kwa Watanzania.

Amesema katika bajeti ijayo, China itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kusaidia miradi inayohitajika kwa haraka katika maendeleo ya nchi, yenye matokeo mazuri katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuongeza ukusanyaji wa kodi.

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

09 Juni, 2017

http://ikulu.go.tz/index.php/media/press_details/4099

Suggset To Friend:   
Print