Mwanzo > Rolling News Report
Dk. Salim kufundisha China
2014-07-04 20:52

SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China, imemualika aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) ambayo sasa ni Umoja wa Afrika (AU), Dk Salim Ahmed Salim, kwenda jijini Beijing kwa ajili ya kufundisha vijana juu ya mapambano ya uhuru katika nchi za Afrika.

Dk Salim, ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa China Li Yuanchao aliyekuwapo nchini kwa ziara yake ya kikazi ya siku sita.

"Nimefurahishwa na mualiko huu na nitachukua fursa hii kwenda kutekeleza nilichoombwa, lakini pia nimeona ni muhimu kuwafundisha vijana wa taifa letu kutambua jitihada za nchi yao na uhusika wa Tanzania katika mapambano ya uhuru Afrika," alisema.

Aidha Dk Salim alizungumzia namna nchi za Afrika zilivyochangia na kusaidia bega kwa bega bara la Asia kurejesha kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN), mchakato ulioanza tangu mwaka 1960 na kumalizika mwaka 1971 na sasa nchi ya China ni ya pili kwa utajiri na ndio inayoongoza chombo hicho cha UN.

Alisema katika kipindi cha vita baridi nchi ya Marekani ilijaribu kuizuia China isishike nafasi yeyote katika chombo hicho cha UN.

"Kwa kuizuia China isiingie UN, ilikuwa inamaanisha kuwa zaidi ya watu milioni 600, walikuwa hawawezi kusaidiwa na chombo hicho, ndipo waafrika tulipoamua kuingilia na kusaidia," alisema.

Katika hatua nyingine Dk Salim, amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kuitazama kwa upana zaidi fursa ya soko la bidhaa la China.

Amewataka kuuza katika soko hilo bidhaa zilizoongezwa ubora ili kunufaika kwa kupata fedha zaidi na kusisitiza kuwa nchi hiyo ni moja ya nchi zenye masoko mazuri kwa bidhaa za hapa nchini.

Kwa upande wake Li, alimpongeza Dk Salim kwa uongozi wake mzuri wakati akiwa OAU na kusema nchi yake itaendelea kumkumbuka kutokana na mchango wake kwenye harakati za ukombozi.

Alisema Dk Salim alifanya kazi kubwa katika kutetea mataifa ya Afrika kuhakikisha yanakuwa huru na kupata haki stahili mbele ya jamii ya kimataifa.

"Kazi ya Dk Salim ilikuwa kubwa hasa katika kupigania haki za wanyonge, aliweza kusimama imara mbele ya Umoja wa Mataifa (UN), na kutetea kundi la walio wengi na wenye haki," alisema.

 

Imeandikwa tarehe 30 Juni 2014

By Halima Mlacha

Habari Leo

Suggset To Friend:   
Print